Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana leo Bungeni Dodoma amesema “Kipekee kabisa, napenda kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Rais Samia, kwa juhudi zake kubwa za kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia programu ya Tanzania – The Royal Tour ambayo imeanza kuleta matunda kwa kuvutia Watalii na Wawekezaji kutembelea nchini ambapo Mawakala wa Utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwemo Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea Tanzania kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao”
“Vilevile Wawekezaji kutoka Taifa la Bulgaria wameonesha nia ya kuwekeza nchini kwa kujenga hoteli nne (4) zenye hadhi ya nyota tano (5) katika hifadhi za Taifa Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Serikali pia imesaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya utalii, biashara na uwekezaji baina ya Tanzania na Jiji la Dallas Marekani, mwezi Aprili, 2022, hatua ambayo itafungua fursa za usafiri wa anga kwa kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Dallas, Marekani na kuongeza idadi ya Wageni nchini”
0 Comments