Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wizara ya Maliasili yaomba bilioni 624

 Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi bilioni 624,142,732,000 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya sekta ya Maliasili na Utalii kwa mwaka ujao wa fedha. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana

Akisoma bajeti hiyo Waziri Balozi Dkt. Chana amesema wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 inatarajia kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 2,500 katika hifadhi za Taifa za Arusha, Burigi - Chato, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Udzungwa, Manyara, Rubondo, Rumanyika - Karagwe, Ruaha, Mikumi, Nyerere na Serengeti.

Aidha, Wizara itajenga njia za utalii zenye urefu wa kilomita 251 na barabara za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 342.5.

Waziri Chana ameongeza kuwa Wizara hiyo itawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 30 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Nyerere na vijiji 18 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Serengeti, kuchimba mabwawa mapya nane na kukarabati mabwawa matano kwa matumizi ya wanyamapori katika hifadhi za Taifa za Mkomazi, Tarangire, Mikumi, Katavi, Ruaha, Saadani, na Serengeti.

"Wizara itaboresha maeneo ya malisho ya wanyamapori kwa kudhibiti mimea vamizi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 30,331 katika hifadhi za Taifa Nyerere, Saadani, Serengeti, Arusha, Ibanda-Kyerwa, Mto Ugalla, Mikumi, Mkomazi na Katavi, vilevile, Wizara itaotesha miti ya asili 100,000 katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro," amesema Balozi Chana.