Ad

Biskuti Za Bangi Zazusha Hofu



Wakati Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikiendelea kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo, taarifa za kuwapo kwa biskuti za bangi maarufu ‘edibles marijuana’ zimezusha hofu kwenye jamii.

Hofu hiyo inatokana na bidhaa hizo kuzalishwa katika baadhi ya viwanda vidogo vya kutengeneza mikate, keki na mchanganyiko wa bidhaa zenye ladha mbalimbali za nafaka vilivyopo hapa nchini.

Mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha keki na biskuti jijini Dar es Salaam alisema licha ya wao kutotengeneza bidhaa hizo, kuna uwezekano baadhi ya viwanda vinatengeneza kwa tamaa ya kujipatia kipato kwa njia haramu.




Taarifa ambazo Mwananchi imezipata ni kuwa bidhaa hizo hutengezwa kwa mchanganyiko wa vitu vingi, ikiwamo mayai, maziwa, unga wa ngano na siagi ili kuweka ladha inayovutia kwa mtumiaji.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameitaka Serikali kuwa macho na kuwachukulia hatua kali watengenezaji wa bidhaa hizo ili kunusuru jamii, hasa vijana ambao ndio wateja wakubwa.


Wakizungumza na Mwananchi, walisema kama kusipokuwa na udhibiti kuna hatari vijana wengi wakatumbukia kwenye matumizi ya bangi hivyo Taifa kupoteza nguvu kazi muhimu.

Mwananchi imepata taarifa kuwa kila kipande huuzwa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000.

Juzi Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerlad Kusaya aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa mpaka sasa wamekamata watuhumiwa wawili wa kuuza na kutengeneza biskuti zenye bangi ndani yake.“Tumemkamata Abdulnasir Komba (30) mkazi wa Kaloleni, Arusha akiwa na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa bangi akiziuza kwenye maeneo hayo, pia tunamshikiria Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha anayesadikiwa kuwa mtengenezaji wa biskuti hizo,” alisema.

DCEA imethibitisha biskuti hizo kuwa ni hatari baada ya kujiridhisha na vipimo vya Mkemia Mkuu wa Serikali vilivyoonyesha madhara yanayosababisha saratani ya koo na shingo, utasa, kuharibu mishipa ya ubongo na via vya uzazi.



Hata hivyo, baadhi ya watu wanaozitumia wameliambia Mwananchi kuwa wanapendelea kuzitumia kwa sababu hazina harufu, hivyo si rahisi kujulikana tofauti na wanapovuta bangi.

Takwimu za bangi

Taharuki za kuwepo kwa biskuti zenye bangi nchini inakuja wiki chache baada ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kupitia ripoti yake ya ‘Tanzania in figures 2021’ kuonyesha ongezeko la kesi na matumizi ya dawa za kulevya nchini, ikiwemo bangi kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na 2022.

Ripoti hiyo inaonyesha kesi za dawa za kulevya zimeongezeka kwa asilimia 25 kutoka kesi 429 mwaka 2020 hadi kesi 537 mwaka 2021.

Makosa ya kukutwa na kutumia bangi yameongezeka kutoka 5,903 mwaka 2020 hadi 7,593 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 28.6, huku mashamba ya bangi yakiongezeka kutoka 27 hadi 85.

Wasemavyo wanafunzi

Mwananchi lilizungumza na baadhi ya wanafunzi wa vyuo jijini Dar es Salaam waliokiri kutumia bangi kwa muda mrefu, lakini sasa wameamua kugeukia biskuti hizo.

Wanasema hutumia biskuti hizo bila kugundulika kwa sababu hazina harufu.

“Hii naitumia kisha naingia darasani na hakuna mwalimu anayeweza kunigundua,” alisema mmoja wa wanafunzi hao aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.

James Kimario (si jina halisi) aliyedai kuwa muathirika wa matumizi ya bangi, alisema kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa anatumia biskuti zinazompa furaha, uchangamfu na amani.

George Mnali, aliyekuwa rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi ya Elimu ya Juu (Tahliso) kati ya mwaka 2018/19 alisema katika kipindi cha uongozi wake, alibaini baadhi ya wanafunzi kutumia kutokana na uhuru waliokuwa nao.


“Watumiaji ya bangi wamekuwa wakijificha, ndiyo sababu wengi wameingia kuanza kutumia biskuti hizo, hii ni hatari, kwani vyuo ndio tumaini la wazazi bora, viongozi na jamii bora, nashauri Serikali ichukue hatua za haraka kudhibiti mtandao wa uzalishaji wa biskuti hizo.”

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Faustine Bee anasema hana taarifa ya matumizi ya biskuti hizo chuoni.



Naye Agnes Msami, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha kusaidia vijana wenye uraibu wa dawa za kulevya Manispaa ya Temeke (MKIKUTE) anasema wanafunzi wengi wa sekondari katika manispaa hiyo wamekuwa waathirika wa matumizi ya bangi.

“Tunapokea waraibu wastani wa 150 kwa siku, asilimia 80 ni umri miaka 20 hadi 40. Hizo biskuti, keki tunasikia zinatumika zaidi vyuoni na tulitamani kupeleka elimu huko, lakini kwa sasa tunafikiria kufika kwenye sekondari za Temeke kwanza,” alisema Agnes.

Baadhi ya wachumi wanasema hali hiyo inaweza kuendelea kuakisi pia matokeo ya utafiti wa hali ya nguvu kazi nchini mwaka 2021, yanayoonyesha asilimia tatu ya kushuka kwa ushiriki wa nguvu kazi katika kipindi cha miaka minane kutokana na sababu mbalimbali.

Dk Donald Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Repoa anasema kiuchumi hali hiyo inaongeza kundi la utegemezi katika jamii, inachangia gharama za matibabu zisizokuwa na ulazima, inapunguza ushiriki wa nguvu kazi katika shughuli za kiuchumi nchini.

“Kama hao watakuwa hawafanyi kazi maana yake uzalishaji unashuka, kiwango cha Pato la Taifa (GDP) kinapungua kwa mwaka, hata makadirio ya mgawanyo wa pato la mtu mmoja unapungua, kwa hiyo ni muhimu sana kushughulikia changamoto hiyo isiendelee kuathiri nguvu kazi,” anasema Dk Mmari.





Source: Mwananchi

Post a Comment

0 Comments